;

Urithi wa kihistoria: Uhusiano usio na utulivu kati ya Kenya na Afrika Kusini

Mnamo mwaka wa 1997, ndege ya Nelson Mandela ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, na zulia jekundu lilikuwa tayari limetandazwa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya wakati huo, Kalonzo Musyoka, alikuwa amesimama akisubiri katika joto kali. Lakini Mandela hakushuka kwenye ndege.

Maafisa wa Afrika Kusini, wakiwa na aibu iliyoonekana wazi, walieleza kwamba Rais alikuwa amelala baada ya safari ndefu kutoka Misri.

Miaka miwili baadaye, tukio kama hilo lilijirudia. Ndege ya Rais Thabo Mbeki ilitua Nairobi. Zulia jekundu tena liliwekwa. Waziri mwingine wa Kenya akasubiri chini ya ndege.

Msemaji wa Mbeki, Parks Mankahlana, kwa mujibu wa gazeti la South Africa la Independent Online (IOL), alishuka kutoka kwenye ndege kuomba radhi, akieleza kwamba Rais alikuwa amefanya kazi hadi alfajiri akisimamia upatanishi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na alikuwa amechoka sana kushuka kwenye ndege.

Ndege hiyo ilijaza mafuta na kuondoka kuelekea Libya kwa mkutano maalum wa Shirika la Umoja wa Afrika (OAU) ambalo sasa linajulikana kama AU.

Hakukuwa na nia mbaya, walisisitiza maafisa wa Afrika Kusini kwa vyombo vya habari, wakieleza kuwa haya yalitokana tu na uchovu. Kenya haikutoa malalamiko ya wazi, lakini tukio hilo liliacha doa, ingawa serikali ya Moi ilielewa kwa nini yalitokea.

Mtaalamu Emmanuel Kisiangani baadaye alitaja matukio haya mawili kama ushahidi kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili haukuwa mzuri kikamilifu, licha ya kuanzishwa kwa uhusiano rasmi wa kidiplomasia mwaka 1992.

Sababu yake, wachambuzi wamekuwa wakibainisha kwa muda mrefu, inatokana na historia ya nyuma Zaidi, Kenya kutoa uungwaji mkono hafifu kwa harakati za ukombozi wa Afrika Kusini, na kuendelea kushirikiana kibiashara na kisiasa na serikali ya ubaguzi wa rangi (apartheid) wakati wapigania uhuru wa Afrika Kusini walikuwa wakipoteza maisha kwa ajili ya demokrasia.

Mzigo huo wa kihistoria haujawahi kuondoka kikamilifu. Kila kilichofuata; taarifa za kirafiki, ziara za viongozi wa nchi, makubaliano ya visa, na miito ya mshikamano wa Kiafrika… yote yamejengwa juu ya msingi ambao haujawahi kuwa imara kikamilifu.

Kenya na Afrika Kusini kwa muda mrefu zimeelezea uhusiano wao kwa maneno ya upendo na heshima kubwa. Taarifa za pamoja za kidiplomasia huzungumzia udugu wa Afrika, maono ya pamoja ya bara, na kuheshimiana kati ya nchi mbili zenye uchumi mkubwa Afrika.

Lugha ya kidiplomasia imekuwa thabiti, iliyopambwa, lakini mara nyingi haioneshi hali halisi iliyo chini yake. Na hali halisi yenyewe ni ya kuvutia zaidi.

Dirisha la wazi zaidi la kuelewa undani wa uhusiano huu lilionekana kupitia nyaraka za siri za ubalozi wa Marekani zilizovuja mwaka 2008.

Wanadiplomasia wa Marekani walizungumza na Tom Amolo, ambaye wakati huo alikuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, na ambaye pia aliwahi kuwa Balozi wa Kenya Pretoria kwa zaidi ya miaka sita, hivyo kuelewa uhusiano huo kwa undani wa kipekee.

Amolo aliielezea Afrika Kusini kama “mshindani anayejitokeza kimkakati” wa Kenya. Alisema uhusiano wao kwa ujumla ni wa kirafiki, lakini urafiki huo una mipaka.

“Huwa wanaweka vizuizi vya kibiashara haraka wanapotuona tunakuja,” aliwaambia Wamarekani mjini Nairobi. “Hata hutumia ushawishi wao kikanda kuwakatisha tamaa wengine kufanya biashara nasi.”

Serikali ya Kibaki ilijibu kwa kuamua kuimarisha uwepo wake wa kidiplomasia nchini Afrika Kusini.

Iliamua kuongeza idadi ya wanadiplomasia walioko Pretoria na, kwa maneno ya Amolo, “kuhakikisha kwamba ni wabobezi na walio bora zaidi, kama Rais alivyoagiza.”

Ahadi ya kufungua ubalozi mdogo Jijini Johannesburg ilitolewa. Lakini karibu miongo miwili baadaye, ubalozi huo bado haujawahi kuwepo.

.

RELATED NEWS