;
Kinara wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka ametoa onyo kali kwa wanasiasa wanaokiuka msimamo wa chama, akisema wanajikatia tiketi ya kwenda nyumbani. Haya yanajiri wakati Kalonzo anajiimarisha kama mgombea urais wa Muungano wa Upinzani akiwa makini kuhakikisha ngome yake imesalia na nidhamu ya kisiasa.
Kizungumkuti kinachomkabili ni kuwa taifa linapojiandaa kwa uchaguzi mkuu wa mwaka ujao Kalonzo ana uhakika wa uungwaji mkono wa wabunge 12 tu kati ya wote 22 kutoka eneo pana la ukambani. Katika kaunti ya Machakos wabunge sita kati ya wote nane wamemtema kwa sababu tofauti zikiwemo baadhi yao kuunga mkono serikali ya Kenya kwanza na wengine kuhisi malengo yao katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao yakihujumiwa kwa kumuunga mkono Kalonzo na chama chake cha Wiper.
Wabunge Caleb Mule wa Machakos mjini, Fabian Kyule wa Kangundo, Joshua Mwalyo wa Masinga na Vincent Musyoka wa Mwala ni wafuasi sugu wa serikali ya Kenya kwanza na ambao wanaongoza kampeni za kuimarisha umaarufu wa rais William Ruto katika kaunti hiyo ya Machakos. Mbunge wa Yatta Robert Basil naye ni wa hivi punde kutajwa kuwa kibaraka wa serikali ya Kenya kwanza aliyeishi kujificha ndani ya chama cha Wiper.
Katika ziara ya muungano wa upinzani kaunti ya Machakos wiki jana Basil alikosa khhudhuria Kalonzo akionekana kutumia maneno makali kumrejelea alipohutubia wakazi wa soko la Matuu lililoko katika eneobunge la Yatta analoongoza Robert Basil. Mbunge wa Mavoko Patrick Makau naye amekua akicheza mchezo wa paka na panya wakati wa ziara za Kalonzo ukambani mara chache anayojitokeza akionekana kusisitiza chama cha Wiper kuandaa uchaguzi wa mchujo angalau kuona ikiwa atashinda tiketi ya chama hicho ili kuwania ugavana wa Machakos katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, ndoto inayofifia kila kunapokucha.
Kalonzo vilevile amepoteza uungwaji mkono wa wabunge watatu kati ya wote nane katika kaunti ya Kitui. Tatu hao ni Rachael Nyamai wa Kitui Kusini, Nimrod Mbai wa Kitui Mashariki na Charles Nguna wa Mwingi magharibi ambaye ni wa punde kuasi chama cha Wiper anachoongoza Kalonzo Musyoka
Wabunge hawa kuendelea kumpigia debe rais William Ruto ni pigo kwa Kalonzo hasa Rachael Nyamai na Nimrod Mbai ambao wana ufuasi dhabiti ikizingatiwa wamekua wakiwabwaga wawaniaji wa chama cha wiper debeni. Hata hivyo ni afueni kwa Kalonzo akipata uungwaji mkono wa wabunge 5 kati ya wote 6 wa kaunti ya Makueni. Mwengi Mutuse wa Kibwezi magharibi ndiye mbunge pekee aliye mamlakani anayempigia debe rais William Ruto katika kaunti ya Makueni. Kutokana na idadi hii ya Wabunge 10 kuwa upande wa rais Ruto, Kalonzo ametaja wabunge hao kama wabinafsi na wanaopea kipau mbele matakwa yao badala ya kuipa jamii nafasi hiyo.
Amewahimiza wapiga kura katika kaunti hizo tatu za Ukambani Kitui, Makueni na Machakos kutowachagua wabunge hao katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao ili hilo kuwa funzo kwao.